Friday, July 28, 2017

JINSI YA KUISHI KAMA NDEGE WA ANGANI


JINSI YA KUISHI KAMA NDEGE  WA ANGANI


“Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

Ndege wa angani hawalimi, hawavuni ila wanakula na maisha yao yanasonga mbele. Na wewe unaweza kusema kwamba kumbe hakuna haja kubwa ya kuhangaika na kuweka juhudi kwa sababu hata nisipofanya hivyo bado nitakula na kuishi. Inasikitisha kuona kwamba dhani hii ya kuishi kama ndege ipo bado katika fikra za baadhi ya watu makanisani.


Ndege wa angani hawalimi, hawavuni ila wanakula na maisha yao yanasonga mbele. Je, nasisi hatuna haja ya kuhanganika kwasababu bado tutakula kula na kuishi tu kwa neema za Mungu?

Katika Mathayo 6:26 tunasoma hivi,

“Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?”

Kufikiria kwamba kifungu hiki kinatupa uhuru wa kukaa bure na kusubiri maisha yaendee yenyewe kwa neema ya Mungu hivyo kutoweka juhudi kubwa kwenye kile tunachofanya ni makosa makubwa.Ukitafsiri hivyo basi wewe umepotoka kwa sababu kuna mambo mengi sana ambayo hao ndege huwa wanayafanya ambayo unatakiwa kuyafanya na huyafanyi.

MAMBO USIYO YAJUA KUHUSU MAISHA YA  NDEGE



Ndege ni viumbe hai wenzetu ambao tumekuwa tunawaona ni viumbe wa kawaida tu lakini wana somo kubwa la kutufundisha. Japo viumbe hawa hawawezi kuongea na sisi moja kwa moja, ila vitendo vyao vinaonesha wazi wazi na hivyo mtu unaweza kujifunza na kuboresha maisha yako sana.

Ingawa Andiko hilo linaeleza upande mmoja tu wa ndege kula bila kufanya kazi na kulishwa na Baba wa Mbingu lakini kuna upande wa pili ambao umefichika. Ndege hao mpaka wapate chakula ambacho Baba wa Mbinguni anawapa kuna mambo mengi sana wanayakabiliana nayo.Hivyo na wewe unayetaka kukaa tu na kulishwa kama ndege lazima uwe tayari kuyapitia ili ufanane nao.

Mambo matano(5) ya kujifunza toka kwa ndege Ambayo hufanya kabla ya                                    kulishwa chakula :

Kwa kuangalia huu mfano wa ndege ambao hawalimi ila wanakula tutajifunza na kuona ni jinsi gani ndege ni waerevu kuliko wewe. Haya utayojifunza yatakusukuma zaidi na kukufanya uamue kuyachukua maisha yako kwenye mikono yako na kuwajibika nayo.


1. Ndege ni watafutaji chakula chao hakitokei kwenye kiota chao bali kinatafutwa:

Ni kweli ndege halimi, wala havuni na kukusanya ghalani lakini pia chakula chao hakitokei pale pale kwenye kiota chao. Ni lazima watoke wakatafute na hata kwenye kutafuta hawakutani nacho kirahisi tu. Wanapitia mazingira magumu sana, wengine wanakoswa koswa kuliwa na Wanyama wengine na ndege wanaokula ndege, wengine wanakoswa koswa kuwindwa lakini wanachukua hatari yote hiyo ili wapate chakula.

Sasa wewe unayetaka kuishi kama ndege lakini haupo tayari kuchukua hatari yoyote ili kuboresha maisha yako basi umepotoka. Unajaribu kufanya kazi fulani kidogo na ukiona hatari unakimbia haraka sana na kukata tamaa. Ndege haishi hivyo.Hapa ni sawa na ndege akoswe na mwindaji siku moja na aseme sitaenda tena kutafuta chakula, nakaa hapa kwenye kiota changu tu. Jifunze somo hili;



Kama unataka mabadiliko kwenye maisha yako ondoka hapo kwenye kiota chako leo. Kama utaendelea kungangania hicho kiota jua hakuna kitakacho badilika.Kiota chako ni hali yoyote ambayo imekuridhisha kwa sasa. Hali ambayo inakufanya uogope kuchukua hatua kwa kudhani ni hatari mno. Maisha yote ni hatari hivyo usiogope kufanya jambo ambalo ni muhimu kwako kwa sababu unaogopa kushindwa.


2. Ndege wana amka mapema asubuhi mwanga ukishatoka na kuanza kutafuta chakula.


Saa kumi na moja na nusu asubuhi tayari utawasikia ndege wanalia huko nje. Hivi umewahi kukuta ndege amelala mpaka saa mbili? Sawa, hata wewe huwa hulali mpaka saa mbili, labda nikuulize hivi tena. Umewahi kukuta ndege amelala mpaka saa mbili kwa sababu siku hiyo ni siku ya jumapili? Au siku ya sikukuu?

Haijalishi ni siku gani kwenye dunia yao, mwanga ukishaonekana tu ndege nao wameamka na wanaendelea na mchakato wao wa kuboresha maisha yako. Sijui kama kuna ndege ambaye huwa anajishauri mara mbili mbili kwamba aamke au asiamke. Na sijui kama kuna ndege ambaye ana alarm anayoweza kuizima na kulala kidogo, dakika tano tu ila anakuja kustuka nusu saa baadae, kama unavyofanya wewe mara kwa mara.

Unakumbuka usemi kwamba ndege anayewahi kuamka ndiye anayepata wadudu wazuri wa kula. Nafikiri hilo halina ubishi, kama kuna mdudu alichelewa kujificha basi ndege anampata kwa urahisi kabisa anapokuwa ameamka mapema. Jifunze somo hili kwa ndege,


Anza siku yako kwa kuamka mapema kila siku, haijalishi ni siku gani. Anza siku yako mapema.
Kuwa na utaratibu wa kuamka mapema kila siku na tumia muda huo kutafakari maisha yako, kupangilia siku yako, kujisomea na hata kufanya kazi zako, kama kazi zako zinawezekana kufanya kwenye muda huo.

Usiache hata siku moja kuamka mapema na usiamke halafu ukaanza kujishauri. Kama unatumia alarm kuamka ikishaita tu, ruka kutoka kitandani na unapoanza kupata mawazo kwamba urudi kulala, jiulize je ndege angefanya hivyo? Kama jibu ni hapana ondoka kitandani na kawahi wadudu wazuri.Wadudu kwako ni zile shughuli muhimu kwako.


3. Hakuna ndege anaye lalamika kwaajili ya hali yake

Sijawahi kuona ndege wa kitajiri, Sasa swali ni je umewahi kumuona ndege wa kitajiri?Yaani ndege ambaye wazazi wake ni matajiri? Na je juhudi zake zinatofautiana na ndege ambaye ni wa kimasikini?


Nafikiri tunakubaliana kwamba hakuna ndege anayekaa chini na kusikitika kwamba leo siwezi kwenda kutafuta chakula kwa sababu wazazi wangu hawajanisaidia. Au ndege analalamika kwamba wazazi wake hawakufanya kitu fulani ndio maana maisha yake sio mazuri. Au ndege anawaambia wazazi wake wampe urithi! Jifunze jambo hili;

Ni marufuku kutoa sababu ya kijinga kama hiyo eti maisha yako sio bora kwa sababu wazazi wako hawakukusomesha, au hawajakupa mali, au ni masikini.Kama umeweza kuwa na akili ya kufikiria hiki, jua kwamba chochote unachotaka kipo kwenye mikono yako.


4. Ndege hawana malalamiko yao kwa serikali.
Labda ndege wana serikali yao, na wana vyama? mimi sijui lakini ninachoweza kusema ni kwamba sijawahi kuona ndege ameacha kwenda kutafuta riziki yake kwa sababu chama chake au serikali imewaahidi maisha bora. Sijawahi kuona ndege ameacha kuweka juhudi kwenye kutafuta riziki yake na kutumia muda huo kulalamika kwamba serikali yao imefanya hiki, mara imefanya kile na kuitumia kama sababu ya kutokupata riziki.

Tunahitaji serikali nzuri lakini hilo sio jawabu la matatizo ya maisha yako.Kama unaamini serikali ndio itakuletea wewe maisha bora umepotoshwa na ukakubali kupotoka.Kama unaamini serikali ndio jibu la matatizo yako umepotoka pia. Lakini mbona niliahidiwa maisha bora na kuhakikishiwa hivyo? Sawa uliahidiwa, je umeyaona maisha hayo bora/ Maisha bora yapo kwenye mikono yako.

Usidanganyike kwamba kuna serikali itakuja kukuletea wewe ugali ukiwa umekaa unabishana au kusifia kwamba serikali ni nzuri. Hivi unajua serikali inakutegemea wewe ndio iende. Yaani wewe usipofanya kazi hakuna mshahara wa kumlipa Raisi.Tunahitaji serikali nzuri lakini hilo sio jawabu la matatizo ya maisha yako.


5. Ndege ni wajasiriamali.

Sijui kama kuna ndege mmoja ambaye ameajiri ndege wengine au kuna ndege ambao wameajiriwa na matumaini yao yote wameweka kwa yule ndege aliyewaajiri.Ndege wanajua juhudi zao ndio zitafanya maisha yao yaendelee kuwepo. Kuna Somo kubwa la kujifunza hapa;

Ajira ni sehemu ndogo sana ya mafanikio ya maisha yako. Unahitaji kuweka juhudi nyingi binafsi ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako. Kama unafanya kile tu ambacho umeajiriwa kufanya na wakati mwingine unafanya kwa kiwango cha chini sana, umekwishapotea.


Nimetumia mfano huu wa ndege ili tuweze kujifunza mambo haya matano muhimu sana kwenye maisha yako. Ndio ndege ni kiumbe mdogo sana, huwezi kumlinganisha na sisi binadamu, sawa kabisa, je kwa hayo anayofanya hajakuzidi maarifa? Hebu anza kuyafanyia kazi hayo mara moja na yafanyie kazi kila siku kama wanavyofanya ndege halafu uone kama maisha yako yataendelea kuwa kama yalivyo sasa.

Pastor Mtitu.

No comments:

Post a Comment

KANUNI 21 ZA KIBIBLIA ZA UTOAJI

Kanuni 21 Za Jinsi Ya Kumtolea Mungu Mungu anatutarajia tumtolea katika mali na mapato yetu( Fedha zetu) anayotubariki,lakini tuna mtolea...