Tuesday, July 11, 2017

KUCHELEWA KWA MUNGU

Kuchelewa Kwa  Mungu

Pengine unakabiliana na jaribu la kuona Mungu anachelewa.Kuna jambo ambalo umekuwa unamtarajia Mungu kulifanya katika maisha yako na bado halija tokea.Na unafikiria na kuwaza lini Mungu atalifanya ? Mbona amechukua muda mrefu? Unajiuliza kwanini Mungu hajajibu maombi yako?

Njia moja wapo ya Mungu kuongeza imani zetu ni kwa kuchelewa kwake kutujibu wakati tunapitia magumu ya maisha na mahangaiko katika maisha.

Tena na tena katika Biblia Mungu anatutia moyo kutokata tamaa nakuacha.Bali kuendelea kumtazama Mungu.Natambua kwamba yupo pamoja nawe unapomngojea na kumsubiri atende. Sio tu anaiongeza imani yako lakini yupo anaufanyia kazi mpango wake.Hivyo omba Mungu akusaidie kungojea kwa subira.

MAOMBOLEZO 3:25-26

Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo. Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu. 

Ni vigumu sana kwetu kusubiri Uongozi wa Mungu.Tunataka tuombe Mungu atupe uongozi wake wa nini tufanye na tunataka jibu lije mara hiyo hiyo.Tujifunze kumsubiri Mungu kwaajili ya baraka zake na uongozi wake.Yeye anajua kila kitu na anao mpango mahususi kwaajili ya maisha yetu.Tujitahidi tuwezazo kukwepa kuharakisha na kumzidi Mungu.

Zaburi 27:14
Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana

Watu wengi hawapendi kusubiri.Mara nyingi utaona huwa tunakataa tamaa na kuvunjika moyo katika kusubiri iwe ni kwenye foleni ya chakula au kusubiri kwenye foleni ya magari,Mara nyingi tuna haraka ya kupata nafasi inayofuatia au kitu kinachofuatia.Mtazamo huu mara nyingi tumeubeba hata katika maisha yetu ya kiroho,tunataka kuharakisha kupata Baraka,kupata majibu ya maombi ,kupata kitu fulani kikubwa n.k

Lakini sasa wakati sisi tuna haraka,Mungu mwenye hata haonyeshi kuwa na haraka.Maandiko yanasema yeye simwepesi katika kufanya mambo,hata katika hasira yeye si mwepesi.Inaonyesha Mungu mara zote huwa na mpango na kusudi kwa kila jambo.

Tatizo na kusuburi ni kwamba sisi hatuna taarifa na maelezo yote.Kwa mtazamo wetu,tunaona kama kila kitu kipo tayari na tunataka Mungu atende ndani ya muda wetu tuliojiwekea,hatujui kwamba Mungu anatenda kwa kufuata mpango na kusudi lake.


“Majibu ya haraka yanatoa manufaa yasiyo na kina”.

Ni kwa nadra sana Mungu hufanya vitu kwa kufuata muda wetu tuliouweka,na kwasababu hii ni rahisi sana kwetu kuvunjika moyo.Kama sio waangalifu,tunaweza kufikiri hatujali au ametukasirikia sisi.

Kusubiri ni sehemu ya maisha  na moja ya vitendea kazi vya Mungu kwa kuwaendeleza watu wake kiroho.

Katika Injili tunao hili likitokea kwa kina Martha na Mariamu wakati ule wana msubiri Yesu aje kumponya Kaka yao,Lazaro ambaye alikuwa ni Rafiki ya kipenzi.Hatimaye Yesu alipotokea,alilaumiwa kwa kuchelewa na kuchukua muda mrefu pamoja na kupewa taarifa. Yerusalemu na Bethania ni umbali wa kilomita kumi tu hivyo haikuwa ingia akilini kwanini amechelewa mpaka siku ya nne ndipo anatokea.

Mara zote Mungu huwa anasababu ya kutufanya tusubiri.Kusubiri ni sehemu ya maisha na ni moja ya zana zake anazotumia kuwaendeleza kiroho watu wake.Biblia imejaa hadithi za watu wa Mungu ambao walipaswa kumsubiri Mungu,watu kama kina Nuhu,Ibrahimu, Musa,Yusufu,Daudi,Yesu,Paulo na wengine wengi wasio hesabika.

Mtu asikudanganye wakati mwingine Mungu atasubri mpaka ni usiku wa manane,muda ukiwa umeendelea sana ndipo atende

Kwa kujifunza maisha ya watu hawa wakuu,tunaweza gundua na kujifunza sababu za Mungu kutufanya tusubiri .

ISAYA 40:29-31

Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;  bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Meinrald A. Mtitu
LIGHT OF HOPE TEACHING MINISTRIES


No comments:

Post a Comment

KANUNI 21 ZA KIBIBLIA ZA UTOAJI

Kanuni 21 Za Jinsi Ya Kumtolea Mungu Mungu anatutarajia tumtolea katika mali na mapato yetu( Fedha zetu) anayotubariki,lakini tuna mtolea...