Saturday, July 1, 2017

NGUVU YA KUONA MBALI KAMA TAI

NGUVU Ya kuona mbali KAMA TAI
Ni wale watu wenye ( maono) uwezo mkubwa wa kuona mbali ndio hufanikiwa kuruka juu sana na kufika mahali pa kutimiza ndoto, malengo na makusudi waliyo nayo katika maisha”
Tai ana sifa nyingi za kipekee zinazomtofautisha na ndege wengine.Moja ya sifa nyingine muhimu inayo mtofautisha  na ndege wengine na  kumfanya aitwe “mfalme wa anga” ni pamoja na nguvu na  uwezo wake mkubwa wa kuona mbali akiwa angani.

Katika Kitabu cha Ayubu sifa hii ya tai kuwa na mcho makali yenye nguvu ya kuona mbali imetajawa ,na tunasoma hivi; “Je, tai hupaa juu kwa amri yako na kujenga kiota chake mahali pa juu? Huishi juu ya miamba mirefu na kukaa huko usiku, majabali yenye ncha kali ndiyo ngome yake. Kutoka huko hutafuta chakula chake, macho yake hukiona kutoka mbali…” 
( Ayubu 39-27-30)

“Tai ana uwezo mkubwa wa kuona mbali  tofauti na ndege wengine
Tai ana uwezo mkubwa wa kuona mbali anaporuka juu angani,katika jicho lake ana maeneo mawili ya kutazamia hivyo ana uwezo wa kuona mbele na kuona kwa upande kwa wakati mmoja.Jicho lake ni kubwa kama la binadamu lakini ukali wake wa kuona ni mara nne zaidi ya mtu mwenye macho mazuri!
Tai ana nguvu ya kubwa sana ya kuona mbali anaweza kuona mpaka umbali wa maili 25 akiwa juu sana angani.Tai anaweza kuruka kwenye mwinuko wa futi 15,000, na uwezo wa kuyaona mawindo katika eneo la kilomita za mraba 1.5 akiwa katika eneo moja,huu ni uwezo mkubwa sana!

Umuhimu wa kuwa na  Maono katika    maisha yetu
Kama  Tai alivyo kuwa na uwezo mkubwa wakuona mbali tofauti na ndege wengine, hivyo  ndivyo ambayo Mtu anayetaka kufakiwa kutimiza kusudi lake la maisha  anapaswa kuwa na Maono. Huwezi kufanikiwa kama huna uwezo  wa kuona mbali,yaani kuwa na maono katika meneo mbalimbali ya maisha yako.

Nabii Habakuki anaandika hivi kuhusu maono, 

Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa,  inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.” (Habakuki 2:2-3 )

Pengine tuanze kwa kujiuliza swali la msingi,Maono ni nini? je ,ninawezaji  kuwa na maono juu ya maisha yangu? Watu wengi wana ndoto  kubwa lakini hawazigeuzi kuwa maono na kuwa na umbo  la kushikika ambapo unaweza kufanya kitu nayo.

Maono ni ndoto inayoingizwa  katika utendaji.Maono ni hatua ya juu ya ndoto,yenyewe huwa dhahiri.Maono ni bayana ,yapo wazi nini unaona mbeleni na nini unafanya sasa kufanikisha hilo .Hakuna kitu kinakuwa na nguvu  mpaka kimekuwa dhahiri. Ukubwa wa maono yako utaathiri kwa moja kwa moja jinsi ugumu wa kuyakamilisha utakavyokuwa.

 “Kama  Tai alivyo kuwa na uwezo mkubwa wakuona mbali tofauti na ndege wengine hivyo hivyo ndivyo unavyopaswa  kuwa na maono tofauti na watu wengine

Rick Warren anasema hivi, “Kinyume na maoni maarufu ya wengi,Maono yakiwa makubwa ,ndivyo ilivyo rahisi kuyafikia.Mara nyingi maono madogo ni magumu sana kwasababu hakuna mtu anaye hamasika nayo.Watu wana hamasika ma maono makubwa.Maono makubwa ni rahisi kuwahamasisha na kuwapa watu changamoto”.

Maono ni ndoto inayoingizwa  katika utendaji.Yapo dhahiri na bayana na yanaweka wazi nini unaona mbeleni na nini unafanya sasa kufanikisha hilo

Maono makubwa ni kama sumaku kubwa,yanavuta watu wengi.Ukitaka kuwashirikisha watu ni bora uwape changamoto kwa malengo makubwa na sio malengo madogo.Ukubwa wa maono yako utaamuliwa na ukubwa wa Mungu wako. Mungu wako ataamua ukubwa wa malengo yako.
Unafikiri Mungu wako ni mkubwa kiasi gani? Suala si wewe unafikiri ni nani,lakini unafikiri Mungu wako ni Nani? Usijifunge katika ndoto zako na kusema “ Nini ninaweza kufanya”

Kuelewa vema  maana ya Maono
Maoni ni ile picha uliyonayo katika macho ya ufahamu wako.Maono tunayo zungumza hapa si yale ya kutokewa na picha fulani halisi ,hasha. Maono  ni hali ya kujua unakokwenda ni ile picha ndani yako ya kile kitakachokuwa mwishoni au baadaye, Hivyo maono ni ule uwezo wa kuona mbele na kutambua ule mwisho utakavyokuwa.

“Kama tai anavyo tofautishwa na ndege wengine kwa uwezo wake mkubwa wa kuona mbali kadhali maono yetu ndio yanayo tutofautisha na watu wengine.”

John Maxwell anayaeleza maono namna hii ;“Maono ni picha uliyonayo katika macho ya ufahamu wako inayoonyesha jinsi mambo yatakavyokuwa au yanavyopaswa kuwa katika siku za usoni. Maono ni taswira ya mambo yanavyotakiwa kuwa siku za baadaye. Picha hii ni ya ndani ya mtu na ya kibinafsi.” 
Anaendelea kufafanua kwamba:“Hatimaye, utapaswa kuichora taswira hii ya akilini ndani ya wengine kama unatamani maono hayo yatimie katika huduma yako. Kama ambavyo Mungu ametumia fikra zako kuunda muonekano huo wa baadaye, itakubidi wewe pia kuwasaidia wengine kukamata maono hayo ndani yao – ili waweze kushiriki katika kuyatekeleza.

Maono  ni hali ya kujua unakokwenda ni ile picha ndani yako ya kile kitaka chokuwa mwishoni au baadaye

Wapo watu wengi wanaochanganya kati ya maono na malengo, haya ni mambo mawili tofauti japo yanategemeana. Maono ni matokeo ya mwisho wakati malengo ni hatua unazoziweka ili kufikia mwisho.Huwezi kuweka malengo bila ya kuwa na maono kwanza.


Mambo Saba Muhimu Kuhusu Maono

1.      Maono  ya Kimungu yanazaliwa katika kutenga muda na Mungu
 Mungu ndiye ambaye anapanda mbegu ya maono ndani yako. Mungu anapofunua maono kwako yanakuja katika namna ya mbegu na ni lazima yakue ndani yako. Mwanzoni maono yanaweza yasiwe wazi sana, yanaweza yasieleweke kwani huwa bado hayajaumbika kikamilifu bado.
Mara nyingi watu wanaopata maono toka kwa Mungu huwa wametumia muda mwingi naye katika maombi kuabudu, ukimya, faragha na kutafakari. Muungano huu hutoa nafasi kwa Mungu kuongea na kufunua yale anayotaka mtu afanye .
Mfano mzuri ni Nehemia ,alipata maono na mzigo wa kuwenda Yerusalemu kujenga ukuta wa mji baada ya kuwa na muda wa kutosaha wa  kujitenga katika maombo( Nehemia  1:4)

2.      Maono hutupa mwelekeo wa maisha yetu, bila maono maisha haya na mwelekeo
Bila uwezo wa kuona mbali maisha ya tai ni magumu,hawezi kupona, ni ule uwezo wake wa kuoana mbali ndio unao mfanya kula mawindo hai “ fresh”.
Kadhalika ni kweli kwetu,bila kuwa na maono mahususi juu ya nini tunaona kinaenda kutendeka siku zetu za usoni,maisha yetu yatakuwa ni magumu na yasiyo na mwelekeo.Hatuwezi kukamilisha mambo fulani katika maisha bila ya kuyaona kwanza kabla katika picha ya ufahamu wetu.Tunapaswa kuwa na maono juu ya maisha yetu katika nyanja mbalimbali.

Hatuwezi kukamilisha mambo fulani katika maisha bila ya kuyaona kwanza kabla katika picha ya ufahamu wetu.

Maono yanatufanya tuwe jasiri kwenye uelekeo sahihi,bila maono watu hupotea na kuangamia.Mtu mmoja alisema hivi ikiwa hujua wapi unako kwenda basi njia yoyote itakufikisha huko.Bila ya maono dhahiri tutapoteza  rasilimali tulizonazo  kama vile muda,fedha,vipawa na watu .
Katika MITHALI 29:18  tunasoma hivi kuhusu maono, “Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.( SUV)” au “Mahali pasipo na maono, watu huangamia, bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.”( NIV)
Maswali haya ni muhimu kujiuliza.Kama hakutakuwa na kufanya kazi tena katika maisha yako,ungetumia muda wako kufanya nini badala ya kufanya kufanya kazi? Maisha yako yatapofika mwisho, jambo gani unafikiri utajuta kutolifanya, kutoliona au kutolikamilisha? Ukishindwa kujibu maswali haya maana yake huna maono na maisha yako.

3.      Hakuna Mtu asiyeweza kuwa  na maono kama akiamua.
Kila mtu anaweza kuwa na maono juu ya maisha yake kama akiamua.Mtu aliye maskini kabisa na wakuhurumiwa kabisa sio yule asiye na pesa,si yule asiyena kiwanja,sio yule asiye na nyumba au magari,si yule asiye na mashamba n.k.Bali ni yule asiye na maono yeyote katika maisha yake!
Mtu maskini kabisa ni yule ambaye hana taswira au picha yeyote katika ufahamu wake inayo onyesha jinsi mambo yatakavyo kuwa na yanavyopaswa kuwa katika siku zake za usoni.

Maisha yako yatapofika mwisho, jambo gani unafikiri utajuta kutolifanya, kutoliona au kutolikamilisha?
Maono ya mtu ni picha yake halisi ya siku za mbele.Maono binfasi yenye ufanisi lazima ya jumuishe mambo yote muhimu ya maisha yako ,Nani unataka uwe,nini unataka kufanya,jinsi gani unataka ujisikie,nini unataka  kumiliki na mengineyo.
“Ingawa maono yako yanakusaiidia kuiona kesho yako,lakini lazima uishi katika wakati uliopo yaani leo. Maono ni tamko la wewe ni nani na nani utakuwa,ni mchakato wa kutengeneza maisha yako.Maono yako ni wapi unaelekea, jinsi gani unafika kule ni kusudi lako,mambo unayoyafanya sasa.”  John G. Maxwell.

4.      Kile Kinacho mtofautisha mtu aliyefaulu na aliyeshindwa kufaulu ni Maono.
Wakati mwingine kinacho mtofautisha mtu aliyefaulu au kufanikiwa katika eneo fulani na mtu aliyeshindwa au kutofaulu ni maono tu.
Maono ni tamko la wewe ni nani na nani utakuwa,ni mchakato wa kutengeneza maisha yako.
E. Parl Hovey amewahi kusema maneno haya kuhusu maono:“Ulimwengu wa mtu kipofu umefungwa na ukomo wa kugusa kwake. Ulimwengu wa mtu mjinga umefungwa na ukomo wa ufahamu wake Ulimwengu wa mtu mkuu umefungwa na ukomo wa maono yake”.

5.      Maono huchukua muda kutimia hivyo yanahitaji uvumilivu:
Maono yanahitaji uvumilivu  mkubwa. Maono yanatufanya macho yetu yabaki kwenye kitovu hata pale ambapo tunavutwa na mambo mengine.Watu wakuu waliokuwa na maono walilazimika kusubiri kwa uvumilivu.
Ibrahimu naye alisubiri kwa miaka 25 kabla ya ndoto yake ya kupata mtoto kutimia. Yakobo alisubiri maiaka 20 kabla hajabarikiwa.Yusufu alililazimika kusubiri kwa miaka mingi kabla ya maono yake  ya kuwa mkuu kati ya ndugu zake kutimia.

6.      Maono yanahitaji kuwashirikisha watu sahihi   katika wakati sahihi.
Unahitaji watu wengine wa kukusaidia kufika pale unapohitaji,hivyo unawahitaji watu wengine. Unawaitaji watu wengine ili ufanikiwe. Kuna watu wana uwezo kuliko wako, watu wanaoyajua mambo mengine kuliko wewe, unauhitaji msaada wao.Watafute watu ambao mtashirikiana, watu wa kukushauri pale unapotaka ushauri.
“Ni watu wachache sana waliofanikiwa peke yao, wengi wamefanikiwa kwa sababu walitengeza timu bora.”
Neno "kampuni" kwa kingereza "company" linatokana na maneno ya kilatin " cum" na " pane" yanayomaanisha " kuumega mkate kwa pamoja".Biashara yako, kazi yako itafanikiwa sio kwa sababu ya wazo zuri ulilonalo bali watu bora wanaokuzunguka.
Katika kushirikisha maono yako si kila mtu anafaa na si kila wakati unafaa.Unapaswa kuwashirikisha watu sahihi na katika wakati sahihi.Yusufu ni mfano wa mtu aliye pata upinzani na matatizo makubwa kwa kushirikisha ndoto yake kwa watu wasio sahihi.Si kila mtu anakubaliana na kufurahia ndoto yako,wengine watataka kuiua ndoto yako,wengine wata kuonea wivu,wengine watakuchukia kwasababu tu ya ndoto yako.

7.      Maono hukabiliana na vipingamizi na upinzani katika safari yake ya kutimia.
Hakuna maono yasiyo na upinzani.Kila mtu mwenye maono atakutana na upinzani fulani katika safari yake ya kutimiza maono yake.Upinzani unaweza kuja kwa sura nyingi.Watu wengine wanaweza wasiyaelewe na kuyatafsiri vibaya maono yako. Kuwa naweza kuwa na upinzani wa kifedha juu ya maono yako au rasilimali nyingine za kuwezesha maono yako kutimia.

Pst.Meinrald A.Mtitu.

1 comment:

KANUNI 21 ZA KIBIBLIA ZA UTOAJI

Kanuni 21 Za Jinsi Ya Kumtolea Mungu Mungu anatutarajia tumtolea katika mali na mapato yetu( Fedha zetu) anayotubariki,lakini tuna mtolea...