Friday, July 28, 2017

JINSI YA KUISHI KAMA NDEGE WA ANGANI


JINSI YA KUISHI KAMA NDEGE  WA ANGANI


“Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?

Ndege wa angani hawalimi, hawavuni ila wanakula na maisha yao yanasonga mbele. Na wewe unaweza kusema kwamba kumbe hakuna haja kubwa ya kuhangaika na kuweka juhudi kwa sababu hata nisipofanya hivyo bado nitakula na kuishi. Inasikitisha kuona kwamba dhani hii ya kuishi kama ndege ipo bado katika fikra za baadhi ya watu makanisani.


Ndege wa angani hawalimi, hawavuni ila wanakula na maisha yao yanasonga mbele. Je, nasisi hatuna haja ya kuhanganika kwasababu bado tutakula kula na kuishi tu kwa neema za Mungu?

Katika Mathayo 6:26 tunasoma hivi,

“Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?”

Kufikiria kwamba kifungu hiki kinatupa uhuru wa kukaa bure na kusubiri maisha yaendee yenyewe kwa neema ya Mungu hivyo kutoweka juhudi kubwa kwenye kile tunachofanya ni makosa makubwa.Ukitafsiri hivyo basi wewe umepotoka kwa sababu kuna mambo mengi sana ambayo hao ndege huwa wanayafanya ambayo unatakiwa kuyafanya na huyafanyi.

MAMBO USIYO YAJUA KUHUSU MAISHA YA  NDEGE



Ndege ni viumbe hai wenzetu ambao tumekuwa tunawaona ni viumbe wa kawaida tu lakini wana somo kubwa la kutufundisha. Japo viumbe hawa hawawezi kuongea na sisi moja kwa moja, ila vitendo vyao vinaonesha wazi wazi na hivyo mtu unaweza kujifunza na kuboresha maisha yako sana.

Ingawa Andiko hilo linaeleza upande mmoja tu wa ndege kula bila kufanya kazi na kulishwa na Baba wa Mbingu lakini kuna upande wa pili ambao umefichika. Ndege hao mpaka wapate chakula ambacho Baba wa Mbinguni anawapa kuna mambo mengi sana wanayakabiliana nayo.Hivyo na wewe unayetaka kukaa tu na kulishwa kama ndege lazima uwe tayari kuyapitia ili ufanane nao.

Mambo matano(5) ya kujifunza toka kwa ndege Ambayo hufanya kabla ya                                    kulishwa chakula :

Kwa kuangalia huu mfano wa ndege ambao hawalimi ila wanakula tutajifunza na kuona ni jinsi gani ndege ni waerevu kuliko wewe. Haya utayojifunza yatakusukuma zaidi na kukufanya uamue kuyachukua maisha yako kwenye mikono yako na kuwajibika nayo.


1. Ndege ni watafutaji chakula chao hakitokei kwenye kiota chao bali kinatafutwa:

Ni kweli ndege halimi, wala havuni na kukusanya ghalani lakini pia chakula chao hakitokei pale pale kwenye kiota chao. Ni lazima watoke wakatafute na hata kwenye kutafuta hawakutani nacho kirahisi tu. Wanapitia mazingira magumu sana, wengine wanakoswa koswa kuliwa na Wanyama wengine na ndege wanaokula ndege, wengine wanakoswa koswa kuwindwa lakini wanachukua hatari yote hiyo ili wapate chakula.

Sasa wewe unayetaka kuishi kama ndege lakini haupo tayari kuchukua hatari yoyote ili kuboresha maisha yako basi umepotoka. Unajaribu kufanya kazi fulani kidogo na ukiona hatari unakimbia haraka sana na kukata tamaa. Ndege haishi hivyo.Hapa ni sawa na ndege akoswe na mwindaji siku moja na aseme sitaenda tena kutafuta chakula, nakaa hapa kwenye kiota changu tu. Jifunze somo hili;



Kama unataka mabadiliko kwenye maisha yako ondoka hapo kwenye kiota chako leo. Kama utaendelea kungangania hicho kiota jua hakuna kitakacho badilika.Kiota chako ni hali yoyote ambayo imekuridhisha kwa sasa. Hali ambayo inakufanya uogope kuchukua hatua kwa kudhani ni hatari mno. Maisha yote ni hatari hivyo usiogope kufanya jambo ambalo ni muhimu kwako kwa sababu unaogopa kushindwa.


2. Ndege wana amka mapema asubuhi mwanga ukishatoka na kuanza kutafuta chakula.


Saa kumi na moja na nusu asubuhi tayari utawasikia ndege wanalia huko nje. Hivi umewahi kukuta ndege amelala mpaka saa mbili? Sawa, hata wewe huwa hulali mpaka saa mbili, labda nikuulize hivi tena. Umewahi kukuta ndege amelala mpaka saa mbili kwa sababu siku hiyo ni siku ya jumapili? Au siku ya sikukuu?

Haijalishi ni siku gani kwenye dunia yao, mwanga ukishaonekana tu ndege nao wameamka na wanaendelea na mchakato wao wa kuboresha maisha yako. Sijui kama kuna ndege ambaye huwa anajishauri mara mbili mbili kwamba aamke au asiamke. Na sijui kama kuna ndege ambaye ana alarm anayoweza kuizima na kulala kidogo, dakika tano tu ila anakuja kustuka nusu saa baadae, kama unavyofanya wewe mara kwa mara.

Unakumbuka usemi kwamba ndege anayewahi kuamka ndiye anayepata wadudu wazuri wa kula. Nafikiri hilo halina ubishi, kama kuna mdudu alichelewa kujificha basi ndege anampata kwa urahisi kabisa anapokuwa ameamka mapema. Jifunze somo hili kwa ndege,


Anza siku yako kwa kuamka mapema kila siku, haijalishi ni siku gani. Anza siku yako mapema.
Kuwa na utaratibu wa kuamka mapema kila siku na tumia muda huo kutafakari maisha yako, kupangilia siku yako, kujisomea na hata kufanya kazi zako, kama kazi zako zinawezekana kufanya kwenye muda huo.

Usiache hata siku moja kuamka mapema na usiamke halafu ukaanza kujishauri. Kama unatumia alarm kuamka ikishaita tu, ruka kutoka kitandani na unapoanza kupata mawazo kwamba urudi kulala, jiulize je ndege angefanya hivyo? Kama jibu ni hapana ondoka kitandani na kawahi wadudu wazuri.Wadudu kwako ni zile shughuli muhimu kwako.


3. Hakuna ndege anaye lalamika kwaajili ya hali yake

Sijawahi kuona ndege wa kitajiri, Sasa swali ni je umewahi kumuona ndege wa kitajiri?Yaani ndege ambaye wazazi wake ni matajiri? Na je juhudi zake zinatofautiana na ndege ambaye ni wa kimasikini?


Nafikiri tunakubaliana kwamba hakuna ndege anayekaa chini na kusikitika kwamba leo siwezi kwenda kutafuta chakula kwa sababu wazazi wangu hawajanisaidia. Au ndege analalamika kwamba wazazi wake hawakufanya kitu fulani ndio maana maisha yake sio mazuri. Au ndege anawaambia wazazi wake wampe urithi! Jifunze jambo hili;

Ni marufuku kutoa sababu ya kijinga kama hiyo eti maisha yako sio bora kwa sababu wazazi wako hawakukusomesha, au hawajakupa mali, au ni masikini.Kama umeweza kuwa na akili ya kufikiria hiki, jua kwamba chochote unachotaka kipo kwenye mikono yako.


4. Ndege hawana malalamiko yao kwa serikali.
Labda ndege wana serikali yao, na wana vyama? mimi sijui lakini ninachoweza kusema ni kwamba sijawahi kuona ndege ameacha kwenda kutafuta riziki yake kwa sababu chama chake au serikali imewaahidi maisha bora. Sijawahi kuona ndege ameacha kuweka juhudi kwenye kutafuta riziki yake na kutumia muda huo kulalamika kwamba serikali yao imefanya hiki, mara imefanya kile na kuitumia kama sababu ya kutokupata riziki.

Tunahitaji serikali nzuri lakini hilo sio jawabu la matatizo ya maisha yako.Kama unaamini serikali ndio itakuletea wewe maisha bora umepotoshwa na ukakubali kupotoka.Kama unaamini serikali ndio jibu la matatizo yako umepotoka pia. Lakini mbona niliahidiwa maisha bora na kuhakikishiwa hivyo? Sawa uliahidiwa, je umeyaona maisha hayo bora/ Maisha bora yapo kwenye mikono yako.

Usidanganyike kwamba kuna serikali itakuja kukuletea wewe ugali ukiwa umekaa unabishana au kusifia kwamba serikali ni nzuri. Hivi unajua serikali inakutegemea wewe ndio iende. Yaani wewe usipofanya kazi hakuna mshahara wa kumlipa Raisi.Tunahitaji serikali nzuri lakini hilo sio jawabu la matatizo ya maisha yako.


5. Ndege ni wajasiriamali.

Sijui kama kuna ndege mmoja ambaye ameajiri ndege wengine au kuna ndege ambao wameajiriwa na matumaini yao yote wameweka kwa yule ndege aliyewaajiri.Ndege wanajua juhudi zao ndio zitafanya maisha yao yaendelee kuwepo. Kuna Somo kubwa la kujifunza hapa;

Ajira ni sehemu ndogo sana ya mafanikio ya maisha yako. Unahitaji kuweka juhudi nyingi binafsi ili kuweza kufanikiwa kwenye maisha yako. Kama unafanya kile tu ambacho umeajiriwa kufanya na wakati mwingine unafanya kwa kiwango cha chini sana, umekwishapotea.


Nimetumia mfano huu wa ndege ili tuweze kujifunza mambo haya matano muhimu sana kwenye maisha yako. Ndio ndege ni kiumbe mdogo sana, huwezi kumlinganisha na sisi binadamu, sawa kabisa, je kwa hayo anayofanya hajakuzidi maarifa? Hebu anza kuyafanyia kazi hayo mara moja na yafanyie kazi kila siku kama wanavyofanya ndege halafu uone kama maisha yako yataendelea kuwa kama yalivyo sasa.

Pastor Mtitu.

Wednesday, July 19, 2017

ALAMA 15 ZA ROHO MTAKATIFU

ALAMA ZA ROHO MTAKATIFU

Kutokana na utendaji na madhihirisho ya kazi  na huduma za Roho Mtakatifu, imempendeza Baba kwamba Roho Mtakatifu awe na alama zinazo mwakilisha.Alama hizi tofauti zinaweka wazi asili,tabia na kazi za Roho,kama vile ilivyo kwa alama za Yesu Kristo ,Mwana wa Mungu.



Alama 15 Za Roho  Mtakatifu.

  1. ALAMA YA MAJI

 Alama ya hii ya maji  inapotumiwa kwa Roho Mtakatifu inawakilisha juu ya utoaji wake wa uzima unaotiririka unaoleta uahi mpya,pia inawakilisha kazi yake ya kuosha na kusafisha na kuzaa matunda. Maji ni alama ya Roho Mtakatifu kwa maana  ya kuwa mito itatoka ndani yetu baaad ya kubatizwa katika Roho Mtakatifu.(Yohana 7:38,39, 4:4, Zaburi 72:6, 87:7, Isaya 44:3, Kutoka 17:6, I Kor.10:4)

2.ALAMA YA MOTO
Alama hii ya moto inatumika kuonyesha utakatifu wa Mungu ambapo Roho Mtakatifu anahusika kuhukumu na kusafisha na kutakasa kama moto.Roho anashuhudia , kuhakikisha na kuhukumu dhambi. Ubatizo wa Roho huambatana na moto wa kiroho .(Mathayo 3:11, Matendo 2:3, Isaya  4:4, Kutoka 19:18, Malaki 3:2-3, Waebrania 12:29)

 3.ALAMA YA UPEPO AU PUMZI.
Alama hii inaashiria utoaji wa uzima wa   pumzi ya Mungu katika nguvu yake ya kutoa uhai mpya.Hii inasisitiza ukweli kwamba Roho Mtakatifu ni Nafsi isiyo onekana lakini bado athari za utendaji wake zinaweza kuonekana. ( Matendo 2:2, Yohana 3:8;Ezekieli 37:9-10 ,Isaya 40:7)

4. ALAMA YA UMANDE
 Alama hii inaashiria kazi ya Roho Mtakatifu  ya kulifariji na kulichangamsha kanisa. kulifanya liwe hai wakati wote.( Zaburi 133:1-3, Hosea 14:5)

5.ALAMA YA MAFUTA
Alama hii ya Roho Mtakatifu inazungumza juu ya mambo haya yafuatayo;kuwekwa wakfu na Uwezo wa Kimungu wa Roho Mtakatifu,Neema ya upako,Uwepo wake wa Uponyaji, na Mwangazio wa mafundisho yake.Ni Roho ambaye huwatia mafuta(kuwateua na Kuwasmika) waamini wa kanisa kwaajili ya kazi za kitumishi. (Luke  4:18, Matendo 10:38, 1 Yohana  2:20,27, Zaburi 23:5

6. ALAMA YA NJIWA.
Alama  ya  njiwa inatumika  kuwakilisha usafi,uzuri,upole, Amani na asili na tabia za Roho Mtakatifu kwa Ujumla.(Mathayo 3:16, Luka 3:22,Mwanzo 1:2, Mathayo 10:16)

 7.ALAMA YA MHURI.
Mhuri ni alama ya umuhimu ya kuonyesha umiliki,na usalama.Alama  hii inasisitiza juu ya kazi ya Roho Mtakatifu ya kututhibitisha mbele za Mungu kwamba Yeye Anatumiliki,tu wake,na ana mamlaka juu yetu na usalama wetu upo kwake. (Efeso 1:13,4:30, 2 Kor. 1:22, 2 Timotheo 2:19)

8.ALAMA YA SAUTI NDOGO YA UTULIVU.
Roho  ni sauti ya Mungu ndani ya mtu inayoleta ufunuo wa mapenzi ya Mungu kwake.Mwanzo 3:8, 2 Wafalme 19:11-13

9.ALAMA YA KIDOLE CHA MUNGU.
Roho ndiye anayeonyeshea kidole cha kumshitaki mwenye dhambi ,kumfanya avutwe na kukujisikia mwenye hatia hata kumpelekea ampokee Yesu Kristo kama mtetezi wake(wakili wake) Luka 11:20, Mathayo 12:28

10.ALAMA YA MALIMBUKO.
Malimbuko ilikuwa ni alama ya mavuno kamili yanayokuja, Alama hii inaonyesha vile kazi ya awali ya Roho Mtakatifu ya kuifanya upya roho ya mwamini(kuzaliwa mara ya pili) inapelekea kwenye wokovu kamili na kutukuzwa kwa mwamini mbele za Mungu. Warumi 8:23

11.ALAMA YA DHAMANA
Dhamana Ni malipo ya mwanzo yanayo ashiria malipo kamili yatakayafuatia.Alama hii  ni kuonyesha vile Kazi ya Roho katika wokovu wetu ni sehemu ya mwanzo ya kazi kamili na kuu ya ukombozi utakao kuja.Alama hii inafanana na ile ya malimbuko. (Efeso 1:13-14, 1Kor. 1:22)

12.ALAMA YA VAZI AU KUVIKWA
Alama hii ya kuvikwa inamaanisha kumvaa Roho Mtakatifu,yaani Roho kuwa juu ya mtu.Ubatizo wa Roho Mtakatifu ni kama kuvaa vazi la kiuungu kutoka juu.Ni vazi la mwamini kwaajili ya huduma mbele za Bwana. (Luka 24:9,Waamuzi 6:34, Isaya 61:10,)

13.ALAMA YA NAMBA SABA.
Namba saba inatumika kuhusisha ufunuo wa Roho Mtakatifu,Ni alama ya ukamilifu,kukamilika ,na kamili,Inawakilisha ukamilifu wa utendaji wa Roho katka ulimwengu. Taa saba,Macho saba,pembe saba,Roho saba . (Ufunuo 1:3-4,4:5,5:6)

  14.ALAMA YA NURU
Roho ni Nuru.Taa saba hizi ni alama za Mwangazio,ufunuo,na uvivio wa Roho Mtakatifu. Macho  saba , Macho saba ni alama ya kuona, ufahamu,kupambanua,Akili, Hii ni ishara wa Roho wa kujua yote, ukamilifu wa kuona na kufahamu yote.( Ufunuo 1:3-4,4:5,5:6)Tunapozaliwa upya nuru huja ndani ya mtu wa ndani kwasababu Roho wa Mungu huingia ( 2 Wakorintho 4:6 Zekaria  3:9,4:10)

15.ALAMA YA NGUVU AU UWEZO.
Pembe Saba ni alama ya nguvu na ulinzi, zinawakilisha uwezo wote,Roho ana nguvu zote. (Ufunuo 5:6). Roho Mtakatifu ni alama ya nguvu na uwezo utakao juu ndani ya mwamini. ( Matendo 1:8, Luka  34:49)


Pastor & Teacher
Meinrald Anthony Mtitu.

Tuesday, July 18, 2017

UTAPOKUWA TAJIRI KUMBUKA MAMBO HAYA.

Mambo Ya matano ya Kufanya Unapokuwa Umebarikiwa  

Na Kuwa  Na Pesa Nyingi



Utajiri unapaswa kuwa Baraka na sio laana,ukishindwa kufuata maonyo haya utajiri utageuka kuwa laana badala ya Baraka.Kama huwezi mambo haya achana na habari za kutaka  kuwa tajiri maana utajiangamiza mwenyewe.


1.Ukiwa Tajiri Unapaswa Ushinde Tabia Ya Kujivuna


Paulo anaandika kwa kusema moja ya jaribu la kulishinda ukiwa tajiri ni “kujivuna”, au ”kujiona”.

1 Timotheo 6:17
Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie.

Utajiri unatabia ya kuzalisha kiburi,hatusemi kwamba kila tajiri ana kiburi,wapo maskini pia na wana kiburi.Kiburi cha tajiri ni katika vile alivyo navyo,atataka  kuheshimiwa, kutambulikwa, kutofautishwa na wengine ,n.k.
Kadiri unavyokuwa na fedha nyingi na mali nyingi ndivyo unavyopaswa kuomba zaidi kuwa mnyenyekevu. Kama wewe ni tajiri unahitaji wakati wote kujikumbusha kuwa mnyenyekevu mbele za Mungu na watu wengine.


 2.Usiweke Matumaini Katika Mali Zako

I TIMOTHEO 6:17 b
“wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie.”


Pamoja na mali zako usiache kumtumaini Mungu ,hili ni jaribu kubwa sana tuna pokuwa na fedha nyingi na mali nyingi.Ndio maana tusipende tu na kufurahia kuhubiriwa kuwa tutakuwa matajiri,tutapewa upako wa utajiri,lakini wahubiri hawatufundishi juu ya changamoto na majaribu ya kuwa tajiri.Wanatuhubiria  tutakuwa matajiri lakini hawatufundishi tutaishi vipi tukiwa matajiri,mtindo wetu wa maisha utakuwa vipi tukiwa matajiri.

Ni rahisi sana kuwahubiria watu na kuwaombea wawe matajiri lakini ni vigumu sana kuwaambia ukweli uliojificha nyuma ya kuwa matajiri.Hapa Paulo anawaambia ukweli bila kuficha,pia  anasema ukweli juu ya changamoto za utajiri.Ni rahisi sana kutumainia mali zinazo shikika tulizo jikusanyia. Najua fedha zina weza kununua bidhaa na huduma mbalimbali.Fedha ina nguvu sana kiasi ya kwamba ni rahisi sana kudanganyika  kufikiria ya kwamba itaweza kutupatia mahitaji yetu yote na  kutupa ulinzi na usalama.

Fedha inaweza kuwa upendo wetu  wa kwanza.katika hali ya kawaida tunavutwa zaidi kutumainia vile vinavyo onekana kuliko Mungu asiye onekana. Ndio maana tunapaswa kujikumbusha kuenenda kwa imani zaidi kulilo kwa kuona.


     3.Uwe Mtoaji Kwa Ukarimu.

I TIMOTHEO 6: 17- 18

Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

Kinga kubwa  yenye mafanikio  ya huu ugonjwa wa kupenda fedha  ni kutoa kwa ukarimu,weka kiwango  ambacho unataka kujikumiliki,na baada ya kufikia lengo lako ,toa kwa ukarimu kinacho bakia Salia kwaajili ya ufalme wa Mungu,Hapa utakuwa salama kiroho.Moja ya jaribu kuwa ambalo tunapaswa kulikwepa ni kadiri tunavyo pata fedha zaidi na zaidi ndivyo tunavyo jaribiwa kuzitumia kibinafsi kwaaji yetu wenyewe.

      4.Epuka matumzi ya anasa

Mungu hana shida na wewe kuwa na fedha na mali,ana shida na vile unavyotumia fedha yako na mali yako.Yakobo anashambulia kwa matajiri ni vile wanavyotumia utajiri wao,wanavyoishi kwa anasa na kufua fedha kwa matumizi ya anasa.“Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha kama vile katika siku ya karamu.” YAKOBO 5:5 .Neno anasa (spatalao) ni neno la kiyunani lenye kumaanisha anasa iliyopiti kiasi.

LUKA 16:19  Katika habari hii,Tajiri alikuwa anaishi kwa anasa  kila siku wakati Maskini lazaro alikuwa anateseka nje ya geti lake. Ni makosa  kufurahia anasa na kuzuia kile ambacho ni haki ya  wengine au kushindwa kuwasaidia  wengine waliokuzunguka wenye mahitaji. Kwa upande mwingine hatupaswi kwenda kwenye kupitiliza sana na kuwahukumu wakristo kwa kufurahia kazi ya mikono yao

      5. Epuka Kujilimbikizia Mali

Kuna tofauti kati ya kujiwekea akiba na kujirimbikizia mali,ambako ni kunasukumwa na ubinafsi na umimi zaidi .

 YAKOBO 5:1-3
“Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia. Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho.”

Neno kujiwekea hazina  katika lugha ya kiyunani ni thesaurizo, Ni neno linalotupa neno la kiingereza Thesaurus,lenye maana ya mkusanyiko wa maneno.Hapa Yakobo alikuwa anaonya walio matajiri walio na fedha nyingi kuto jirimbikizia vitu.


Yesu anatuona dhidi ya kujilimbikizia fedha na mali katika  Luka 12:15, anasema “Ndipo Yesu akawaambia, “Jihadharini! Jilindeni na aina zote za choyo. Kwa maana maisha ya mtu hayatokani na wingi wa mali alizo nazo.”

Hakuna tatizo kama tunaweka akiba kwa kusudi iliyo halali, Kuchakuri hutunza karanga ili aweze kuwa na kitu cha kula kwa mwaka mzima,chungu,mchwa n.k.Kuweka akiba fedha kwaajili  ya matumizi yasiyotarajiwa ni busara na akili.

Mungu hakubariki ili uhodhi na kulimbikiza,anakubariki ili uwe chanzo cha Baraka zake wa wengine.  - Carlos Wilson


Kuweka akiba kwaajili ya usoni  ni bora kulilo kukopa fedha wakati  utapokuja.Biblia haikatazi kujiwekea akiba na kuweza,lakini ina kuhukumu vikali kujilimbikizia.Kujirimbikizia hakupaswi kuondoa imani kwa Mungu.Watu wanaojilimbikizia mara nyingi hujikuta wanaondoa imani yao kwa Mungu kama mtoaji.

Yesu alionya sana juu ya  kujilimbikizia fedha kibinafsi,.Mungu hatoi utajiri ,mali ili ilimbikizwe bali itumike na wengine.Badala ya kujiwekea hazina Mbinguni kwa kutumia hazina zao kwa manufaa ya wengi walikuwa kwa ubinafsi wanajilimbikizia wenyewe kwa usalama wao na raha zao wenyewe.

Meinrald Mtitu.


Sunday, July 16, 2017

KIONGOZI MTUMISHI

Kiongozi Mtumishi


Falsa ya Yesu juu ya uongozi inasema uongozi ni utumishi,ni kuwa mdogo na mtumishi wa wote.Yesu hakuhusisha kabisa uongozi na Ukuu (Ubosi).Pale wanafunzi wake walipokuwa wanagombania ukubwa aliweka wazi kwamba katika uongozi wa kiroho mambo ni tofauti na vile uongozi wa ulimwengu au wa kawaida ulivyo.

Mathayo 20:25-28
Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Wafuasi wa kwanza wa Yesu walidhania kwamba uongozi unamaanisha Nguvu,nafasi ya heshima na utukufu.Na siku moja wawili miongoni mwao wakaomba nafasi ya mamlaka mmoja kuwa upande wa kushoto na mwingine wa kulia.

1.     Ukubwa sio kuwa juu ya wengine bali kuwatumikia wengine.

Yesu Kristo ni mfano wa kuuigwa wa Kiongozi Mtumishi  ambaye amewahi kuishi hapa duniani  Yeye alitumia tukio kufafanua na kuweza wazi kwa wanafunzi wake wote ni maana ya Ukubwa. Maana ya ukubwa kwa mujibu wa Yesu  ni si kuwa bwana juu ya wengine bali kuwatumikia wengine. “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. (Marko 10:45)

Rick Warren anasema, “Wanafunzi wa Yesu walishindania juu ya nani atachukua nafasi ya juu, na miaka 2,000 badaye, viongozi wa Kikristo bado wanapigania nafasi na kujulikana katika kanisa,madhehebu na huduma shiriki za kanisa.”

 Uongozi wa kiutumishi ni muhimu leo kwasababu kutokuwa na matumaini kuna kuongezeka kwa kasi  kupita kupatika kwa masaada.Watu wanahitaji kuwaamini na kuwategemea viongozi na katika kanuni zinazofanya kazi.

2.     Uongozi ni jukumu la kuwatumikia wengine

Yesu anatoa mfano wa mtindo wa uongozi  alioufundisha pale alipo alipowaosha miguu wanafunzi wake na kuwapa wito wa kufanya majukumu ya kuwatumikiwa wengine ( Yohana 13;12-17).Katika Maandiko  Biblia ambayo Yesu amezungumza kwa uzito sana kuhusu Kiongozi kuwa Mtumishi.

Vile ulimwengu unavyosema kuhusu kiongozi halisi ni yupi ni toafauti kabisa na vile Yesu alivyosema.

Yesu anasema kwamba kuwa kiongozi sio suala la kuwafanya watu wakutumikie,bali uongozi ni suala la kuwatumikiwa wao.Kadiri ninavyo watumiki wengine zaidi,ndivyo Mungu anavyoniinua zaidi katika utumishi.Yesu anasema kama unataka kuwa Mkubwa wa wote,ni lazima ujifunze kwanza kuwa mtumishi wa wote.

MATHAYO 20:26-28
Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Vifungu hivi viwili navitazama kama ndio msingi wa uongozi wa Kikristo.Yesu alifundisha kinyume kabisa na vile ulimwengu unavyosema  juu ya kiongozi halisi ni yupi.Vile ulimwengu unavyosema kuhusu kiongozi halisi ni yupi ni toafauti kabisa na vile Yesu alivyosema. Katika Ulimwengu ili uwe Kiongozi mkuu una jenga piramidi na unapanda juu kabisa.

LUKA 22:24-27
 Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye. Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye. 

3.     Kutisha na kutawala wengine kwa nguvu sio Utumishi.

Katika ulimwengu watu wanatafuta kufika juu kabisa kwa kutisha wengine na kuwatawala kwa nguvu.Watu wanatafuta kuwa namba moja kwa gharama yoyote hili na  wapo tayari kuwakanyanga wengine wote ili mradi tu wafike pale juu.Yesu yeye anasema si hivyo,Yule anayetumika  vema ndiye anayeongoza vema.Utumishi ndio uongozi.Kadiri unavyotumika vyema ndivyo Mungu anavyokuinua zaidi katika uongozi.Uongozi ni utumishi.Yesu mwenyewe nasema wazi,”Hakuja kutumikiwa bali kutumika”.Hebu tutamani kuwa viongozi watumishi kama Bwana wetu Yesu.Inasikitisha sana kuona viongozi mabwana wamejaa kila mahali leo ndani ya kanisa.

4.     Moyo wa utumishi ndio msingi wa uongozi

Kuna uwezekano wa kutumika kanisani kwa maisha yote bila kuwahi kuwa mtumishi. Lazima uwe na moyo wa mtumishi. Je, unawezaje kujua kama una moyo wa mtumishi? Yesu alisema, “Unaweza kusema wao ni nani kwa yale wayatendayo.”
Leo utumishi umepoteza maana yake ,Mtumishi wa leo ni bosi,ni mtu wa kunyenyekewa, anaye lindwa na walinzi maalumu waliovalia makoti marefu na miwani mieusi,Yesu hakuwa na mlinzi hata petro alipojitolea  alimvunja moyo kumlinda.Watumishi wa leo ni kujipa majina makubwa makubwa,kujigamba sana ,kujisifu kupita kiasi, kushindanisha utajiri walio nao n.k. Huu sio utumishi alio ufundisha Bwana Yesu.


Meinrald Mtitu.


SHERIA ZA KUPANDA NA KUVUNA-2



SHERIA ZA KUPANDA NA KUVUNA-2

4.Sheria za kupanda na kuvuna zinatenda kazi katika pande zote mbili za mema na mabaya.

Wengi wetu tukisikia juu ya kuvuna tulichopanda, huwa tunafikiria zaidi ni kwa upande ule mbaya.Tunafikiri juu ya kulipia matokea ya matendo yetu ya dhambi au maamuzi ya kijinga tuliyofanya,lakini  Sheria ya kuvuna sio tu kwa upande wa ubaya.Sheria  hizi ni zipo pia kwa upande wa uzuri .Si upande wa hasi tu bali na upande wa chanya.

Sheria hizi  zinafanya kazi kwa yote, mema na mabaya tunayopanda  katika maisha yetu tuta yavuna.

Sheria za kuvuna zipo chanya sana,na zina simama kama ahadi ya braka kwa kupanda yale yaliyo mazuri na wakati huo  huo zinasimama na kuonya kwa yale mabaya yanayopandwa.

Mungu ameweka kanuni hizi katika maandiko ili zitumike kama maonyo  na kama kutia moyo.Katika Wagalatia 6:7 ,Neno lake linasema “ Msidanganyike,kila mtu atavuna kile alichopanda"

Kila mkulima anelewa maana kanuni hii;Tunavuna zaidi kile tunachopanda, na muda wa baadaye zaidi ya ule tuliopanda.
Kwasababu ya watu kuishi maisha ya uzembe na kutojalia na anasa ni kwa sababu wamedanganyika.Hawaamini ukweli,au wanafikiri Sheria za Mungu kwao zitakuwa tofauti. Sheria ya Mungu haina upendeleo inafanya kazi kwa watu wote.
Ahadi  na maonyo ya Maandiko ni kwamba tunavuna kile tulicho panda.Hii ina maanisha kwamba uchaguzi katika maisha umejaa matoke yake yote mazuri au mabaya,ya muda mrefu na milele.Kuvuna kile tulichopanda kuna maanisha tunavuna tu kile kilichopanda,na tena tunavuna kwa aina ile tu tuliyoipanda,na tunavuna katika misimu tofauti na ule tulioupanda,tunavuna zaidi ya vile tulivyo panda,lakini pia tunavuna kwa kadiri tulivyo panda.

Mambo yanayotutokea sisi sasa,ni mavuno ya mawazo na matendo tuliyo panda zamani.Mawazo na matendo ya leo ni mbegu zinatazopandwa kwaajili ya mavuna ya siku  zetu zijazo.

Kupanda na kuvuna ni analojia ,sahihi kabisa ya maisha yetu. NI mfano wa kitu kinachowakilisha maisha yetu.Tutafanya vema kama tutayaona maisha kama ni mchakato wa kupanda mbegu na kuvuna mavuno na kukuwa makini na kile tunacho panda.Kwa kuwa sisi sote sasa tunavuna kile tulicho wahi kupanda wakati fulani na tunapanda kile ambacho tutakuja kuvuna huko mbele,ni vizuri na muhimu sana  kama tutajifunza na  kuzijua kanuni hizi za kupanda na kuvuna.

5.Kuvuna na kupanda ni sheria  ya ulimwengu wa kiroho

Kupanda na kuvuna pia ni sheria ya ulimwengu waroho.Ni zaidi tu ya kanuni ya kilimo.ni uhakika usio hitaji uthibitisho wa maisha kwamba tunavuna kile tulichopanda.Tunawajibika kupanda na Mungu anawajibika kwa Mavuno.Sisi tuwatenda kazi pamoja na Mungu.

Mungu hazalishi kufeli,Yeye ni Bwana wa Mavuno. Kwa sheria hizi ambazo Mungu ameziamuri,tunahitaji kupanda mbegu ambazo zitaleta matunda sasa na milele.Yeye ni Bwana wa Mavuno. Kila tunapoingia katika msimu mpya lazima tuanze na kupanda.
Kupanda na kuvuna Ni zaidi tu ya kanuni ya kilimo ,ni sheria pia ya ulimwengu waroho.
Katika Luka 6:38,Yesu anatuhakikishia kwamba tunaweza kuitumainia sheria hii.Sheria ya kupanda na kuvuna mara zote inafanya kazi,na inafanya kazi kwa namana ile ile kwa kila mtu.Kama utapanda mambo mabaya,utavuna mambo mabaya.



Katika mstari wa 37 anaanza kwa onyo la  “usihukumu”.Jaribu kudhania  nini kitatokea utafanya hivyo,jibu ni wazi utavuna hukumu.Kama utajiepusha na kuhukumu  wengine,utajiepusha na kuvuna hukumu kutoka kwa wengine. Anasema “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. “
Kisha katika mstari wa 38 anaendelea kwa kuonyesha utekelezaji wa sheria wa kupanda na kuvuna katika utoaji  wetu kwa vitu mbalimbali; hivyo ndiyo anavyosema , “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. 
Hii inaizungumiza hofu ya kila mwanadamu,ambayo ,ni kwamba kama nitatoa,sitabakia na kitu kwaajili yangu mwenyewe.Yesu anasema kwamba  kinyume chake ndio kweli.
Toa kile ambacho wewe ndicho unakihitaji sana,na utapata zaidi. Sio tu utakuwa na vya kutosha kwaajili yako,bali kadiri unavyotoa zaidi,ndivyo utavyopewa zaidi. Kadiri upandaji unavyokuwa mkubwa,Uvunaji nao huwa mkubwa.
Kila matendo mazuri,kila tendo la huduma ambalo si la kibinafsi,kila maneno mazuri ya wema,kila nia njema,kila tabasamu la upendo,kila maamuzi ya kusamehe na kusahau, kila maamuzi ya kuwavumilia wengine yatarudia sisi, katika kipimo kizuri, kilicho shindiliwa,kutikiswa na kumwagika.
6. Kupanda na kuvuna ni sheria  ya msingi katika ufalme wa Mungu
Ufalme wote wa Mungu unatendakazi  katika kanuni ya kupanda na kuvuna.Kama unataka kushiriki na kuhusika katika ufalme,ni lazima upande mbegu.Kama unataka kupokea vitu vizuri ambavyo Mungu ameviandaa kwaajili yako,lazima upande mbegu maalumu kwaajili ya mavuno maalumu.
1 Wakoritho 15:3–4.
Ukristo umeanza na Mbegu iliyopana-Jina lake  lilikuwa ni Yesu Kristo.Mungu alimpanda Mwanawe wa pekee na leo hii tumeongezeka na kuzijidisha na kuwa mamilioni mwa waamini wake ambao tunaitwa Wana na mabinti wa Mungu.Mungu alipanda Mbegu ( Mwana wake), na watu wote ambao wameyatoa maisha yao kwa Yesu Kristo ni Mavuno yake.
Marko 4:26–29
Ufalme wote wa Mbinguni unatenda kazi kwenye  kanuni ya kupanda na kuvuna.Kama unataka kujihusisha nao na kushiriki katika Ufalme wa Mungu,nilizama upande Mbegu.Ukitaka kupokea mambo mazuri ambayo Mungu ameyaandaa kwako,lazima upande Mbegu maalumu kwaajili ya  mavuno maalumu.
Sisi Tunawajibika kupanda na Mungu anawajibika kwa mavuno.Tuwatendakazi pamoja na Mungu.Mungu hazalishi kufeli;Yeye ni Bwana wa mavuno.Kwa sheria hizi ambazo Mungu ameziweka katika utaraibu wake,tunahitaji kupanda mbegu ambazo zitakwenda kuleta matunda kote sasa na kwa milele.Yeye ni Bwana wa mavuno.Tunapo ingia kila msimu mpya,ni lazima tuanze kupanda.
Kuzijua kanuni za kupanda na kuvuna itakufanya kuwa makini na maisha yako ukijua kwamba kila siku unapanda mbegu kwa maneno yake,matendo yako na mawazo yako. Kanuni hizi za kupanda na kuvuna ni moja ya ufunguo wa kuona umuhimu wa mabadiliko katika maisha yetu.

Meinrald Mtitu.

KANUNI 21 ZA KIBIBLIA ZA UTOAJI

Kanuni 21 Za Jinsi Ya Kumtolea Mungu Mungu anatutarajia tumtolea katika mali na mapato yetu( Fedha zetu) anayotubariki,lakini tuna mtolea...